Mwanafunzi 77 wahitimu baada ya kupokezwa mafunzo ya kompyuta Saku.
Na JB Nateleng
Wazazi katika Kaunti ya Marsabit wametakiwa kuhakikisha kuwa watoto wao wanapata mafunzo ya kompyuta, hasa baada ya kukamilisha kidato cha nne, ili kuwapa ujuzi wa kidijitali unaohitajika katika ulimwengu wa sasa.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Kituo cha Ebisa Youth Empowerment Center, Abdikadir Doyo Wario, mafunzo hayo yanawalenga kuwapa vijana ujuzi utakaowawezesha kujiajiri pamoja na kujiendeleza kimasomo katika taasisi za elimu ya juu.
Akizungumza katika hafla ya kuwatunuku vyeti wanafunzi 77 waliohitimu mafunzo ya kompyuta katika kituo hicho, mjini Marsabit, Doyo Wario amesema kuwa ujuzi wa kompyuta ni muhimu kwa kila mtu, hasa katika enzi hii ya maendeleo ya teknolojia ya kidijitali.
Aidha, Doyo Wario ameangazia changamoto zinazowakumba vijana katika kaunti ya Marsabit, zikiwemo ukosefu wa ujuzi wa kompyuta wakati wa kutafuta ajira, matumizi ya dawa za kulevya na masuala mengine ya kijamii, akisema hali hiyo ndiyo iliyomchochea kuanzisha mafunzo hayo ili kuwainua vijana.
Ameongeza kuwa mafunzo hayo yanaendana na mipango ya serikali ya kitaifa inayolenga kukuza uwezo wa vijana.
Baadhi ya wanafunzi waliohitimu wamepongeza mpango huo, wakisema utawasaidia wanapoendelea na masomo yao katika vyuo vikuu au taasisi nyingine za elimu ya juu.



Post Comment