Loading Now

Highlights

Wafanyabiashara na bodaboda walalamikia uhaba wa mafuta Marsabit,

Na Nyabande Orwa

Siku chache baada ya serikali kuhakikishia wananchi kuwa kuna mafuta ya kutosha nchini, kaunti ya Marsabit imeanza kukumbwa na uhaba wa mafuta katika vituo mbalimbali vya kuuza mafuta mjini.

Kwa mujibu wa utafiti wa kituo hiki, wafanyabiashara wengi wamekosa mafuta ya petroli, huku dizeli ikiwa bado inapatikana kwa kiasi kidogo.

Kutokana na hali hii, baadhi ya vituo vya mafuta vimeanza kupunguza kiwango cha mafuta kinachouzwa kwa kila mteja ili kuepusha kuisha kabisa.

Wafanyabiashara wa mafuta wanasema uhaba huo unasababishwa na hali ilivyo katika eneo la Moyale, ambapo magari ya uchukuzi hulazimika kuja kujaza mafuta Marsabit. Hali hii imeongeza msongamano mkubwa katika vituo vya mafuta mjini.

Wamiliki wa magari sasa wanahofia kuwa hali inaweza kuwa mbaya zaidi iwapo hata depo zitakosa mafuta. Wameitaka serikali kuweka mikakati ya kudhibiti bei ya mafuta ili kuwasaidia wananchi wa kipato cha chini, hasa wanaotegemea biashara kama bodaboda kujikimu.

Kwa upande mwingine, waendesha bodaboda wamelalamikia kupunguzwa kwa kiwango cha mafuta wanachoruhusiwa kununua katika vituo hivyo. Baadhi yao wanasema hulazimika kusukuma pikipiki zao hadi vituoni wanapokosa mafuta barabarani.

Wametoa wito kwa serikali kuingilia kati haraka ili kutatua tatizo hilo.

Haya yanajiri wakati sakata ya uagizaji wa mafuta nchini ikiendelea kushika kasi.

Post Comment