Loading Now

Highlights

Jamii ya Loiyangalani yatoa msimamo kuhusu usajili wa ardhi ya jamii

Na JB Nateleng

Chama cha Loiyangalani Diaspora Professionals Association kwa kushirikiana na viongozi na wakazi wa wadi ya Loiyangalani na Mount Kulal, kaunti ya Marsabit, kimetoa msimamo wake kuhusu mchakato ujao wa usajili wa ardhi ya jamii katika eneo hilo.

Kupitia barua iliyoandikiwa Naibu Kamishna wa Kaunti Ndogo ya Loiyangalani na ambayo imeonekana na meza ya Radio Jangwani, chama hicho kimesema kuwa jamii imeafikiana kwa pamoja kwamba usajili wa ardhi ya jamii utafanyika kwa pamoja katika ngazi ya wadi, ukihusisha maeneo ya Loiyangalani hadi Moite.

Aidha, jamii imeeleza kuwa inatarajia kupokea mwongozo na taarifa rasmi kuhusu mchakato huo kupitia uongozi wa kaunti ya Marsabit, kwa mujibu wa taratibu za kiutawala.

Wakati huo huo, chama hicho kimesisitiza umuhimu wa kufuata taratibu zilizowekwa na kuwashirikisha wakazi pamoja na viongozi husika ili kuhakikisha mchakato huo unafanyika kwa uwazi na ushirikishwaji.

Hata hivyo, wamewataka wanajamii kuendelea kudumisha amani na mshikamano, huku wakihimiza utulivu na ushirikiano wakati wa utekelezaji wa zoezi hilo.

Post Comment