Highlights

Idara ya afya Marsabit yaahidi kukarabati chumba cha kina mama kujifungua katika zahanati ya Shurr

NA Nyabande Orwa

Waziri wa afya katika kaunti ya Marsabit, Malicha Boru, ameahidi kuwa idara hiyo inashughulikia marekebisho ya chumba cha kina mama kujifungua katika zahanati ya Shurr iliyoko eneo bunge la North Horr.

Haya yanajiri siku moja baada ya wakazi wa eneo hilo kulalamikia hali mbaya ya mazingira katika zahanati hiyo na kudai imetelekezwa.

Akizungumza na Shajara leo Jumatano Waziri Malicha amesema kwa sasa wanangoja taratibu za bajeti kukamilika ili kuanza ukarabati wa kituo hicho kilichojengwa mwaka 2013.

Kwa sasa, amewashauri kina mama wajawazito wanaohitaji huduma za kujifungua kufika katika kituo cha afya cha Jaldesa, kilichoko umbali wa takriban dakika kumi kutoka Shurr.

Aidha Waziri amesema vituo vya afya vya umma katika kaunti hii vina dawa.

Malicha amesema kuwa takriban mwezi mmoja uliopita wizara ya afya iliagiza dawa kutoka shirika la usambazaji wa dawa nchini, KEMSA, na kupokea asilimia 79 ya dawa zote zilizoagizwa.

Waziri huyo ameeleza kuwa aina ya dawa zinazopelekwa katika kila kituo cha afya hutegemea mahitaji ya kituo husika, hali inayosababisha tofauti ya upatikanaji wa dawa katika vituo mbalimbali.

Na kuhusu malalamishi ya wananchi kutoka eneo la Bori eneo bunge la Moyale walioandamana wiki jana Malicha amesema kuwa vituo vya afya katika eneo hilo vinaendelea kutoa huduma ipasavyo.

Post Comment