Wadau waitaka idara ya Elimu ya Chekechea kufuata kanuni za ajira na kuwalinda walimu
NA JB Nateleng
Idara ya Elimu ya Chekechea katika Kaunti ya Marsabit imehimizwa kuwalinda walimu walioajiriwa leo Jumatano kwa kuzingatia kanuni za ajira, hatua itakayosaidia kuinua hadhi ya elimu katika shule hizo.
Akizungumza na wanahabari Meneja Msimamizi wa shirika la World Vision kaunti ya Marsabit James Jarso, amehoji uwepo wa hulka ya kuwapa walimu uhamisho kutoka kituo kimoja hadi kingine bila kuzingatia vigezo hitajika.
Jarso amesisitiza kuwa hulka hiyo inavuruga mpangilio wa elimu katika shule zinazoathirika.
Jarso ameelezea kwamba juhudi za kushinikiza ajira ya walimu wa chekechea zimezaa matunda, hatua itakayo boresha na kuimarisha elimu ya vituo hivyo mashinani.
Kulingana na Jarso kampeni ya kuhamasisha ajira ya elimu wa chekechea ilianza mwezi Machi mwaka jana, ambapo Shirika la World Vision lilishirikiana na wadau wa elimu pamoja na kamati ya elimu katika bunge la kaunti.
Kupitia ushirikiano huo waligundua upungufu mkubwa wa walimu wa chekechea katika shule nyingi jimboni Marsabit.



Post Comment