Vijana waliopata Nyota Fund Marsabit wametakiwa kuchangamkia hatua ya kupewa leseni za biashara bure kwa mwaka mmoja
NA Samuel Kosgei
VIJANA waliofaidi na mradi wa Nyota Fund katika Kaunti ya Marsabit wametakiwa kuchukua leseni za kuanzisha biashara bila malipo, kama alivyoahidi Gavana Mohamud Ali.
Waziri wa Biashara, Jeremiah Ledaanyi, amesema vijana waliopokea ufadhili wa mradi huo wanapaswa kutumia fursa hiyo kuanzisha biashara zao mapema bila kikwazo cha gharama za leseni.
Ameeleza kuwa vijana hao hawatatozwa ada yoyote ya leseni kwa kipindi cha mwaka mmoja ujao, kufuatia agizo la gavana Mohamud Ali alilotoa alipohutubia vijana katika eneo la Archers Post, kaunti ya Samburu.
Kwa mujibu wa Gavana Abshiro, hatua hiyo inalenga kuwapa vijana afueni na kuwainua kiuchumi katika nyakati hizi ngumu za maisha.
Hata hivyo, Waziri Ledaanyi amesema mapato ya ushuru wa ndani wa kaunti bado yako chini ikilinganishwa na kiwango kinachotarajiwa.
Amesema serikali ya kaunti inaweka mikakati madhubuti ya kuhamasisha wafanyabiashara kutambua umuhimu wa kulipa ushuru kwa maendeleo ya kaunti.
Aidha, ameongeza kuwa serikali inapanga kuanzisha mfumo wa kidijitali wa ukusanyaji ushuru ili kuongeza uwazi na kuzuia ufisadi pamoja na ubadhirifu wa fedha za umma.



Post Comment