Wafanyabiashara wadogo Moyale kunufaika na mfumo mpya wa biashara bila ushuru.
NA Samuel Kosgei
Itakuwa afueni kwa wafanyabiashara wadogo katika mji wa Moyale baada ya serikali za Kenya na Ethiopia kusaini mkataba wa kuruhusu wafanyabiashara wa mapato ya chini kuvusha bidhaa zao kupitia kituo rasmi cha forodha bila kulipa ushuru.
Akizungumza na kituo hiki ofisini mwake, Waziri wa Biashara Kaunti ya Marsabit, Jeremiah Ledaany, amesema hatua hiyo itarahisisha biashara za mipakani na kuwazuia wafanyabiashara kutumia njia zisizo halali, hivyo kupunguza ufisadi, usumbufu na gharama zisizo za lazima.
Katika makubaliano hayo ambayo kaunti imehusika kikamilifu, waziri amesema kuwa bidhaa zenye thamani ya chini ya shilingi elfu mia moja thelathini hazitalipiwa ushuru, hatua anayosema inalenga kuongeza mapato ya vijana na wanawake wanaojishughulisha na biashara ndogo ndogo.
Wanaosafirisha bidhaa katika ng’ambo nyingine watafanya hivyo mara nne kwa mwezi, umbali wa kilomita 50 kuingia nchini Ethiopia.
Waziri Ledaany amesema kurahisishwa kwa mchakato huo kutaimarisha usalama wa wafanyabiashara, kupunguza dhuluma hasa dhidi ya akina mama, na kukomesha ulaghai unaowaathiri zaidi vijana wa eneo la Moyale.
Mchakato huu umefanikishwa na wizara ya Biashara, shirika la TradeMark Africa, Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Uswidi – SIDA, kampuni ya Triple Line pamoja na Taasisi ya Sera za Uchumi na Jamii ya Ukanda wa Pembe ya Afrika na washirika wengine.
Ujumbe huo ulikuwa na lengo la kushirikiana na Serikali ya Kaunti ya Marsabit kuanzisha majaribio ya Mfumo Rahisi wa Biashara katika Kituo cha Mpaka cha Huduma za Pamoja cha Moyale (One Stop Border Post)



Post Comment