Afueni kwa watu wanoishi na virusi vya UKIMWI Marsabit Central, serikali ya kaunti ikiwapa msaada wa chakula
NA JB Nateleng
Ni afueni kwa watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI katika kaunti ndogo ya Marsabit Central baada ya serikali ya kaunti ya Marsabit kuwapa chakula cha msaada.
Hatua hii inalenga kuwasaidia kukabiliana na makali ya njaa yanayotokana na athari za kiangazi.
Akizungumza na idhaa hii baada ya kutoa magunia 40 ya mchele pamoja na magunia 20 ya maharagwe kwa kundi hilo, Mkurugenzi wa mawasiliano katika serikali ya kaunti ya Marsabit Dalach Elema, amesema serikali ya kaunti inaendelea kutafuta njia mbadala za kuwasaidia wakaazi kupambana na athari za ukame.
Elema amesisitiza kwamba serikali hiyo inawalenga watu walio hatarini zaidi huku ikiendelea kusaka raslimali za kuongeza misaada wa wakaazi Marsabit.
Mtetezi wa watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI Qabale Tache amepongeza hatua hiyo akisema kuwa msaada huo utawasaidia kupunguza makali ya njaa.
Qabale vilevile ametoa wito kwa serikali ya kaunti kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali ili kuongeza mgao akisema idadi ya wanaohitaji misaada ni kubwa.



Post Comment