Highlights

Kaunti ya Marsabit miongoni mwa kaunti zitakazonufaika na umeme wa nishati ya jua kupitia mradi wa KOSAP

NA Caroline Waforo

Kaunti ya Marsabit ni miongoni mwa kaunti 14 nchini zinazotarajiwa kunufaika na umeme unaozalishwa kupitia nishati ya jua chini ya mradi wa Kenya Off-Grid Solar Access Project, KOSAP

Mradi huo unaotekelezwa na Serikali kuu kwa ufadhili wa Benki ya Dunia kwa kima cha shilingi bilioni 15, unalenga kuboresha upatikanaji wa umeme katika kaunti ambazo hazijaunganishwa na mfumo wa umeme wa gridi ya kitaifa.

Kaunti hizo ni pamoja na kaunti ya Marsabit, Garissa, Mandera, Wajir, Kwale, Kilifi, Taita Taveta, Tanariver, Turkana, Samburu, West Pokot, Narok, Isiolo pamoja na kaunti ya Lamu,

Mradi huo wa KOSAP, unasimamiwa na wizara ya Nishati kwa ushirikiano na Kampuni ya kusambaza umeme nchini KPLC na shirika la umeme mashinani REREC kwa lengo la kuhakikisha wakenya wanapata umeme kwa bei nafuu.

Akizungumza baada ya kikao cha kuhamasisha wanahabari kuhusu mradi huo, afisa wa KOSAP katika kaunti ya Marsabit Gideon Gesile, amesema mradi huo utatekelezwa katika maeneo mbali mbali jimboni kama anavyoeleza.

Maeneo yanayolengwa pia yanatarajiwa kunufaika na miradi mingine katika sekta za afya, elimu pamoja na ile ya maji.

Mradi huo unaotarajiwa kuleta umeme kwa bei nafuu pia unalenga kuchangia katika uhifadhi mazingira kupitia matumizi ya nishati safi.

Kulingana na Gesile, KOSAP pia inalenga kuboresha maisha ya wanawake kupitia uhamasishaji wa matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kutumia majiko maalum hatua inayolenga kupunguza matumizi ya kuni na makaa.

Serikali imesema kuwa mradi wa KOSAP ni sehemu ya juhudu za kufanikisha mpango wa kitaifa wa upatikanaji wa umeme ifikapo mwaka 2030.

Post Comment