Highlights

Wanaharakati wamahamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kuasi dhulma za kijinsia.

Wanaharakati katika kaunti ya Marsabit na maeneo ya jirani wanaendelea kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kupambana na dhulma za kijinsia.

Akizungumza na kituo hiki, Spika wa Bunge la Vijana katika eneo bunge la Saku na mwanaharakati wa shirika la pastoralist youth focus initiative, Abdiaziz Boru, amesema kuwa njia bora ya kukabiliana na dhulma za kijinsia na mila potovu ni kuhusisha jamii nzima katika mabadiliko.

Boru anasema kuwa kupitia hamasa za kina katika kipindi cha siku 16 za uanaharakati inayoanza kila tariki 25 mwezi Novemba hadi Disemba 10, jamii inaweza kupata uelewa mpana na waathiriwa kupata nafasi ya kupona.

Wakati huohuo, mwanaharakati kutoka Kaunti ya Isiolo, Abdikadir Osman, anatoa wito kwa wanaharakati na wadau wengine kuongeza juhudi za kuingia mashinani hasa katika maeneo  bunge ya Saku, North Horr na Moyale. Anasema kina mama pia wanapaswa kuhamasishwa kupitia kliniki mbalimbali ili wapate elimu kuhusu athari za dhulma za kijinsia na jinsi ya kuripoti matukio wanayokumbana nayo.

Osman pia amewataka viongozi wa kidini kuendelea kuhimiza jamii kuachana na mila potovu zinazoathiri wasichana. Aidha, amezisihi serikali za kaunti kushirikiana katika mapambano dhidi ya dhulma za kijinsia kwa kufadhili kampeni na jumbe za kuelimisha jamii kupitia vipindi vya redio.

Osman amezungumza na kituo hiki kwa njia ya simu.

Post Comment