County Updates, Diocese of Marsabit, Local Bulletins

Mbunge Wa Moyale Qalicha Gufu Aitaka Tume Ya NCIC Kumkamata Na Kumshtaki Aliyekuwa Mwakilishi Wa Wadi Ya Torbi, Pius Yatani Kwa Kutoa Matamshi Ya Uchochezi.

Mbunge wa Moyale Qalicha Gufu.
Picha;Hisani

By Jillo Dida Jillo,

Mbunge wa Moyale Qalicha Gufu   ameiomba serikali na tume ya maridhiano ya kitaifa NCIC kumkamata na kumshtaki aliyekuwa mwakilishi wa wadi ya Torbi, Pius Yatani kwa kutoa matamshi ya uchochezi ya kijamii katika kaunti ya Marsabit miaka miwili iliyopita.

Mbunge huyo ameteta kuwa licha ya agizo la polisi kumkamata mwanasiasa huyo, bado hajatiwa mbaroni kutokana na kosa la kutoa matamshi ya uchochezi kutoka Ethiopia hadi Tana River dhidi ya Jamii Oromo.

Akizungumza na Radio Moja humu nchini,  Gufu amemshutumu mwakilishi wadi huyo kwa kuchangia utovu wa usalama katika kaunti ya Marsabit,mzozo ambao umeshuhudiwa kwa muda mrefu.

Kauli hii inajiri siku chache baada ya waziri wa fedha Ukur Yattani ambaye ni mshirika wa karibu wa Pius  kuwashitaki  wanasiasa watatu kutoka kaunti za Marsabiti na Isiolo kwa kumchafulia sifa mwezi uliopita .

Ukur,kupitia kwa wakili wake  G&A Advocates, amewataka mwakilishi wa wanawake wa  Isiolo  Rehema Dida Jaldesa, mbunge wa Saku  Dido Ali Raso na  Qalicho Gufu Wario wa  Moyale  kuomba msahama kwa kosa hilo .

Mbunge huyo pia amesema kuwa hakuna haja ya kuhofia kisa cha maajuzi ambapo bunduki moja ilipatikana ndani ya gari ya serikali ya kaunti ya Marsabit.

Aidha Kalicha amepongeza juhudi za MCA wa Uran Halkano Konso kujisalimisha katika  afisi ya DCI kwa uchunguzi zaidi.

Kaunti ya Marsabit imeshuhudia utovu wa usalama wa mara kwa mara unaoletwa na makundi ya wezi wa mifugo waliojihami kwa silaha.

Subscribe to eNewsletter