County Updates, Local Bulletins

HOSPITALI YA RUFAA YA MARSABIT YASHUTUMIWA KUTOKANA NA MADAI YA KUWAPA WAGONJWA DAWA ZILIZOHARIBIKA.

Na Waandishi wetu.

WATETEZI wa haki za kibinadamu kaunti ya Marsabit wanataka usimamizi wa Hospitali ya rufaa ya Marsabit kuweza kuadhibiwa vikali kutokana na ufichuzi wa kamati ya seneti kuwa huenda wagonjwa wanapewa dawa zilizopita muda wa matumizi.

Wakiongozwa na mtetezi wa haki za kibinadamu kutoka shirika la Centre for Research Rights and Development (CRRD) Mohamed Hassan ameambia shajara kuwa ni kosa la kushtakiwa kwa usimamizi wa hospitali kwa madai ya kupeana dawa zilizoharibika kwa wagonjwa kwani wanahatarisha afya na maisha ya wananchi.

Hassan ameitaka kamati ya seneti kutoa adhabu kwa idara ya afya ya kaunti kwa kuhifadhi dawa zilizoharibika sawa na kuruhusu utumizi wa sanitaiza zilizoharibika.

Aidha Hassan amesikitikia hali ya afya katika jimbo la Marsabit suala analosema serikali ya kaunti imezembea kwani licha ya idara hiyo kuwa nyeti ina bajeti ndogo na hivyo kuchangia upatikanaji wa huduma duni.

Kauli yake inajiri siku chache baada ya kamati ya afya ya seneti kuzuru jimbo la Marsabit, Wajir na Mandera kutathmini hali ya afya kwenye hospitali za umma.

Kamati hiyo ilitembelea Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Marsabit na kukuta mfumo ambao umelemewa na usiosimamiwa vizuri.

Kamati hiyo kwenye ripoti imesema kuwa wanaosaka vipimo vya saratani kila mwezi ya wameongezeka mara dufu, lakini vipimo muhimu vya maabara husafirishwa hadi Nairobi kutokana na ukosefu wa uwezo wa uchunguzi wa ndani.

Vyoo viligundulika havina maji, viti vya wheelchair vikiwa vichafu kati ya nyingine.

Zaidi, wafanyakazi wa hospitali walithibitisha matumizi ya dawa na vitakasa mikono vilivyokwisha muda wake.

Subscribe to eNewsletter