County Updates, Local Bulletins

AFISA WA POLISI, MOYALE, AHUKUMIWA KIFUNGO CHA MIAKA 20 JELA KWA KOSA LA KUMNAJISI MSICHANA WA MIAKA 15.

Na Mwandishi Wetu,

Mahakama ya Moyale imemuhukumu kifungo cha miaka 20 jela afisa mmoja wa magereza mwenye umri wa miaka 31 kwa kosa la kumnajisi msichana wa miaka 15 mara kadhaa katika lokesheni ya Sessi eneo bunge la Moyale kaunti ya Marsabit.

Mahakama hiyo ilimpata na hatia Abdishakur Hassan Hamed baada ya upande wa mashtaka kudhibitisha kuwa kati ya tarehe 1 mwezi Mei na tarehe 30 mwezi uo huo mwaka 2022 katika lokesheni ya Sessi mshtakiwa alimnajisi msichana huyo aliyekuwa katika kidato cha kwanza mara 5 na kumpachika ujauzito.

Hili lilibainika baada ya mamake mwathiriwa kugundua kuwa mwanawe alikuwa na ujauzito miezi sita baadae.

Afisa huyo aliyehudumu katika gereza la Moyale alikamatwa mwezi Novemba na kufunguliwa mashtaka mwezi uo huo mbele ya hakimu katika mahakama ya Moyale Willy Cheruiyot ambapo alikanusha mashtaka dhidi yake.

Baada ya mwathiriwa kujifungua mahakama iliagiza uchunguzi wa msimbojeni yaani DNA kufanyika ambapo ilibainika kuwa afisa huyo alikuwa ndiye babake mtoto wa mwathiriwa.

Mnamo tarehe 25 mwezi uliopita wa Aprili Hakimu Willy Cheruiyot alimpata na hatia afisa huyo na kumhukumu kifungo hicho cha miaka 20 gerezani.

Afisa huyo ana siku 14 kukata rufaa.

Subscribe to eNewsletter