Local Bulletins

Zaidi ya washukiwa 300 wakamatwa huku bunduki haramu zaidi ya 200 zikinaswa kufuatia oparesheni Ondoa Jangili Marsabit, Isiolo

Na Caroline Waforo

Operesheni Ondoa Jangili katika kaunti za Marsabit na Isiolo imefanikisha kukamatwa kwa washukiwa zaidi ya 300 huku zaidi ya bunduki haramu 200 zikinaswa.

Haya ni kulingana na waziri wa usalama wa kitaifa Kipchumba Murkomen aliyezungumza hapo jana wakati wa kikao cha jukwaa la wananchi zamu ya kaunti ya Marsabit.

Waziri amesema kuwa oparesheni hiyo inalenga kukomesha shughuli za majangili wa kundi la OLF kutoka taifa jirani la Ethiopia ikiwemo ulanguzi wa dawa za kulevya pamoja na ulanguzi wa binadamu.

Vile vile waziri amesema kuwa migodi ya Hillo iliyoko lokesheni ya Dabel eneo bunge la Moyale itafunguliwa baada ya mikakati yote ya kiusalama kuimarishwa huku akisema kuwa kupitia operesheni Ondoa Jangili wamefanikiwa kuwaondoa majangili waliokuwa wakiendesha shughuli za uchimbaji haramu wa madini katika migodi hiyo.

Aidha waziri amethibitisha kuwa kati ya washukiwa waliokamatwa ni maafisa wa polisi na hata maafisa katika serikali ya kaunti kwa kufanikisha uchimbaji haramu wa madini.

Haya ni huku taarifa zikisema kwamba bado shughuli zinaendelea katika migodi hiyo nyakati za usiku na kufanikishwa na maafisa wa polisi pamoja na viongozi serikalini.

Waziri Murkomen pia amepongeza amani inayoshuhudiwa jimboni Marsabit baada ya kipindi kirefu cha migororo ya kijamii huku akiwataka wananchi kudumisha amani.

Aidha amewataka wanasiasa katika jimboni kuhubiri amani haswa kuelekea uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2027.

Waziri Murkomen anafanya ziara za kiuslama nchini leo hii akiwa katika kaunti jirani ya Isiolo.

Subscribe to eNewsletter