Local Bulletins

Wavuvi haramu 30 wamekamatwa kwa kuvua samaki kinyume cha sheria ziwa Turkana kipindi cha mwaka moja uliopita.

NA CAROLINE WAFORO

Takriban wavuvi 30 wamekamatwa kwa kuvua samaki kinyume cha sheria katika maeneo yanayolindwa katika ziwa Turkana upande wa kaunti hii ya Marsabit katika kipindi cha mwaka moja uliopita.

Haya ni kulingana na Mkurugenzi mwandamizi wa shirika la Wanyamapori KWS tawi la kaskazini mashariki Gideon Kebati ambaye amezungumza na shajara ya Radio Jangwani afisini mwake.

Wavuvi hao ambao wengi wao ni kutoka kaunti ya Turkana wamefikishwa kortini na hata kuhukumiwa huku Kebati akitoa wito kwa wavuvi kutovua samaki katika maeneo yaliyolindwa.

Kebati amesema kuwa samaki wanapungua katika ziwa Turkana hii ikisababishwa na hatua ya wavuvi kuvua samaki hao kwa kutumia njia zisizofaa kama vile kutumia nyavu zisizostahili.

Na kutokana na kupungua kwa samaki katika ziwa Turkana Kebati anasema kuwa wavuvi hujaribu kuvua samaki katika maeneo yanayolindwa na maafisa wa KWS na kusababisha makabiliano kati ya maafisa wa KWS na wavuvi hao.

Kadhalika Kebati amesema kuwa pana haja kubwa ya kuwa na mpangilio wa soko la samaki huku pia akiwataka kuchukua tahadhari wanapoendelea na shughuli zao za uvuvi.

Subscribe to eNewsletter