Local Bulletins

Waakazi wa Marsabit watahadharishwa dhidi ya mama mmoja anayewahadaa wananchi kwa kuwauzia kuni kutoka msitu wa Marsabit

Na Caroline Waforo,

Tahadhari imetolewa kwa wakaazi jimboni Marsabit dhidi ya kuhadaiwa katika ununuzi wa mbao na kuni kutoka kwa watu wanaodai kuwa maafisa wa idara ya misitu jimboni KFS.

Ni tahadhari ambayo imetolewa na mhifadhi wa misitu katika ukanda wa kaskazini ya juu Mark Leng’uro na ambaye alikuwa mlinzi wa msitu wa Marsabit kabla ya uhamisho wake.

Leng’uro anasema kuwa amepokea malalamishi kutoka kwa baadhi ya wakaazi jimboni Marsabit wanaodai kuhadaiwa na mwanadada moja anayedai kuwa ni mfanyikazi katika idara hiyo ya KFS akidai kuuza mbao haswa kwa taasisi mbalimbali jimboni kama vile shule.

Amesisitiza kuwa lengo la idara ya KFS ni kulinda misitu na wala sio ukataji wa miti.

Leng’uro amesema kuwa serikali kupitia wizara ya mazingira imekuwa ikisisitiza umuhimu wa upanzi wa miche katika taifa ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na kufanikisha mradi wa kupanda miche bilioni 15 ifikapo mwaka 2032.

Mhifadhi huyu wa misitu sasa amewataka wananchi jimboni kuendeleza zoezi la upanzi wa miche ili kutunza mazingira.

Aidha Leng’uro ametoa onyo kwa wafugaji dhidi ya kupeleka mifugo wao katika maeneo yaliyopandwa miche ili kuhakikisha kuwa tunatunza msitu wa Marsabit.

 

 

 

Subscribe to eNewsletter