Local Bulletins

Viongozi wa kisiasa Marsabit waonywa dhidi ya kuingiza siasa kwenye suala la usalama.

Na Carol Waforo

Viongozi wa kisiasa wameonywa vikali dhidi ya uchochezi hapa katika kaunti ya Marsabit. Ni onyo ambalo limetolewa na kamishna wa kaunti ya Marsabit James Kamau ambaye amezungumza na wanahabari ofisini mwake baada ya kuzuru eneo la mkasa ambapo mhudumu moja wa bodaboda aliuawa na wahalifu wasiojulikana kwa kudungwa kisu mara kadhaa.

Mkasa huo ulitokea katika eneo la Arobota lililoko katika lokesheni ya Dakabaricha eneo bunge la Saku kaunti ya Marsabit na ambapo bodaboda yake iliibwa.

Kamishna amewaonya wanasiasa dhidi ya kuhusisha siasa kwenye maswala ya kiusalama katika jimbo hili.

Kamishna Kamau ametoa hakikisho kwa wananchi kuwa uchunguzi utafanyika na waliohusika na mauaji hayo watakamatwa huku akisema kuwa idara ya usalama itawatambua wahalifu wote katika mji wa Marsabit na kuchukuliwa hatua madhubuti. Kamishna ameelezea hofu ya uwepo wa wahalifu humu mjini Marsabit akisema kuwa watashirikiana na washikadau mbalimbali ili kumaliza uhalifu huo.

Aidha idara ya usalama itaandaa vikao na wahudumu wa bodaboda ili kuwa na mazungumzo ya jinsi ya kuendesha shughuli hizi za bodaboda.

Subscribe to eNewsletter