Local Bulletins

Usalama waimarishwa katika eneo la Dukana kaunti ya Marsabit.

Na Caroline Waforo,

Usalama umeimarishwa katika eneo la Dukana eneo bunge la North Horr Kaunti ya Marsabit kufuatia matukio ya utovu wa usalama ya hivi maajuzi mpakani mwa taifa hili la Kenya na lile la Ethiopia.

Haya ni kulingana na naibu kamishna wa eneo la Dukana Charo Katana ambaye amezungumza na Shajara ya Radio Jangwani kwa njia ya simu.

Katana amesema kuwa baada ya matukio hayo idara ya usalama imefanya kila juhudi kurejesha utulivu.

Kulingana na Katana wakaazi katika maeneo yaliyoathirika walikuwa wameshauriwa kukusanyika mahala pamoja ili kurahisisha mikakati ya kuwapa ulinzi.

Vilevile amewahakikishia wakaazi wa Dukana usalama wao akisema kuwa sasa hakuna sababu ya kuwa na hofu yoyote.

Na baada ya wazee wa jamii ya Dukana kutakiwa kuwatambuwa wahalifu waliotekeleza uhalifu katika eneo la Dillo katika taifa jirani la Ethiopia Katana anasema kuwa uchunguzi bado unaendelea.

Haya yanajiri huku mkutano wa amani kati ya jamii za maeneo ya Dukana nchini Kenya na Dillo nchini Ethiopia zikitarajiwa kushiriki mkutano wa amani hapo kesho baada ya mkutano mwingine kuandaliwa Jumatano wiki jana.

Inatarajiwa kwamba maeneo mengine humu nchini pamoja na baadhi ya wilaya nchini Ethiopia zitajumuishwa katika mazungumzo hayo.

Subscribe to eNewsletter