Local Bulletins

Sheria ya kuzuia serikali ya kaunti ya Marsabit kubadilisha miradi ya wananchi ovyo ovyo yachapishwa.

Na Samuel Kosgei

Sheria inayolenga kuhakikisha kuwa pesa za maendeleo ya jimbo la Marsabit haielekezwi kwingine iko tayari kutumika baada ya kuchapishwa kwenye gazeti rasmi la serikali.

Hayo yamesemwa na MCA wa Laisamis Burcha ambaye alikuwa mwasisi wa sheria hiyo iliyoitwa Marsabit County Equitable Development Bill 2024.

Burcha ameambia kituo hiki kuwa mswada huo sasa ni sheria inayosubiri kutekelezwa na serikali ya jimbo huku akitaraji kuwa miradi mingi ya maendeleo za wadi itakayowekwa kwenye bajeti ya 2025/26 itatekelezwa kupitia sheria hiyo mpya.

Amesema ana imani kuwa sheria hiyo itatumika kusawazisha maendeleo kote jimbo bila kubadilishwa kwani tayari gavana wa Marsabit Mohamud Ali aliweka saini kuwa sheria.

Kiongozi huyo ambaye pia ni kiranja wa wengi katika bunge la Marsabit amesisitiza kuwa sheria hiyo itazuia miradi waliopendekeza wananchi kubadilishwa ovyo ovyo.

Kwa muda mrefu anasema kuwa wananchi wamekuwa wakiteta kuhusu miradi waliopendekeza wakati wa  kuundwa kwa bajeti kuhamishwa au kukosa kutekelezwa.

Subscribe to eNewsletter