Local Bulletins

Ofisi ya CDF Laisamis yashtumiwa kwa kutogawa fedha za basari kwa njia ya usawa.

Na Isaac Waihenya,

Ofisi ya hazina ya ustawi wa maeneo bunge CDF Laisamis imeshtumiwa kwa kile ambacho kimetajwa kuwa ni kutogawa fedha za basari kwa njia ya usawa.

Kwa mujibu wa mwanaharakati wa kutetea haki za binadamu kutoka eneo bunge la Laisamis ambaye jina lake tumelibana ametaja kwamba kwa muda sasa hakujakuwa na usawa katika ugavi wa fedha za basari kwa wanafunzi wa eneo hilo huku wanafunzi wengine wakipata shilingi elfu 50,000 na wengine wakipata shilingi elfu 9,000 pekee.

Akizungumza na meza ya habari ya Radio Jangwani kwa njia ya simu, mwanaharakati huyo amelalama pia kuhusiana na kufungwa kwa ofisi za CDF za eneo bunge hilo (ofisi ya Marsabit mjini na ofisi ya Laisamis) kila mara akisema kuwa hilo limelemaza upatikanaji wa huduma kwa wananchi wa eneo bunge la Laisamis.

Amelalama kuwa kufugwa kwa ofisi sawa na kukosekana kwa wafanyikazi wa ofisi hiyo kunalemaza utendakazi.

Hata hivyo mwenyekiti wa CDF katika eneo bunge hilo Bi. Rafaela Neepe amekanusha madai hayo huku akitaja kwamba kumekuwa na usawa katika ugavi wa fedha za basari ispokuwa katika hali za kipekee ambapo anayefadhiliwa ni yatima.

Bi Rafaela amewataka wazazi kuwa na subira kwani kucheleshwa kwa zoezi la ugavi wa fedha za CDF kunatokana na kuchelewa kwa fedha kutoka hazina ya taifa.

Vilevile Bi Rafaela amekanusha madai kuwa ofisi za CDF za eneo bunge hilo (ofisi ya Marsabit mjini na ofisi ya Laisamis) zimefungwa huku akitaja kwamba kuwa katibu huwa ofisin kila mara katika ofisi ya Marsabit japo hakutaja muda kamili ni lini ofisi ya Laisamis itakapofunguliwa.

 

Subscribe to eNewsletter