Supkem Marsabit yaunga mkono wito wa kuwajibisha serikali ya Kenya Kwanza.
December 5, 2024
Na Caroline Waforo
Huku kaunti ya Marsabit ikijiunga na ulimwengu kuadhimisha kampeni ya siku 16 za utoaji uhamasisho na kukomesha dhuluma dhidi ya wanawake wasichana jimboni Marsabit wametakiwa kukumbatia elimu kama moja wapo ya njia za kupambana na dhulma hizi.
Haya ni kulingana na mwakilishi wadi mteule katika bunge la kaunti ya Marsabit Sadia Araru ambaye amezungumza na shajara ya radio jangwani kwa njia ya simu.
Kulingana na Araru iwapo wasichana watawezeshwa kimasomo basi wataweza kutambua haki zao na kujilinda dhidi ya dhulma mbalimbali ikiwemo ndoa za mapema pamoja na ukeketaji wa wasichana.
Mwakilishi wadi huyo amewataka wanawake kuhakikisha kwamba wanajikuza na kujiimarisha kimaisha ili kukomesha tamaduni ya kutegemea waume zao pamoja na kumaliza umaskini.
Ameongeza kuwa changamoto hizi zimewafanya wanawake wengi kukabiliana na matatizo ya msongo wa mawazo.
Sadia pia ametahadharisha jamii dhidi ya kuendelea kushikilia mila na tamaduni zilizopitwa na wakati na ambazo zinachangia katika dhulma dhidi ya wasichana na wanawake.
Vile vile amewarai wazee wa jamii pamoja na wazazi kuwa katika mstari wa mbele katika kukomesha dhulma hizi.
Kupotoka kimaadili, tamaduni, gharama ya juu ya maisha pamoja na matatizo ya kiakili ni moja wepo ya mambo ambayo yametajwa kuchangia katika kuongezeka kwa visa vya dhulma dhidi ya wanawake ikiwemo mauaji ambayo yameendelea kushuhudiwa humu nchini.
Kampeni hiyo ya kila mwaka ya kupigania haki za wanawake ilianza hapo jana Novemba 25 ambayo ilikuwa ni siku ya kimataifa ya kukomesha dhuluma dhidi ya wanawake, hadi Disemba 10 ambayo ni siku ya haki za binadamu. Kampeni hii inaambatana na kauli mbiu ya mwaka huu ikiwa ni kuungana kukomesha dhuluma dhidi ya wanawake.