Local Bulletins

Amani yatangazwa Marsabit baada ya wazee wa jamii za Gabra na Borana kuafikia kukomesha mapigano

By Mark Dida

Washukiwa sita wakuu wa mapigano ya kikabila baina ya jamii za Gabra na Borana wamesema wameamua kuleta amani na maridhiano kufuatia mazungumzo.

Wakiwahutubia waandishi wa habari katika kikao cha pamoja hapa Marsabit, viongozi hao walikiri kuwa wameafikiana haya wakiwa wamefungiwa kwa siku saba ndani ya seli ya polisi hapa Marsabit.

Mwenyekiti wa baraza la jamii ya Borana Guracha Boru amesema lengo la maafikiano yao ni kurejesha tena umoja na mshikamano baina ya jamii hizo.

Guracha ameongezea kuwa nia yao ni kwa pande zinazozozana kuungana na kuweka silaha chini ili kuruhusu mazungumzo zaidi kufanyika bila hata kuhusisha wanasiasa au asasi za kiusalama.

Kauli ya Guracha imekaririwa na aliyekuwa mwakilishi wa Turbi/Bubisa ambaye pia ni mzee wa jamii ya Gabra Pius Yattani.

Aidha Yattani ametahadharisha vijana kuwa makini kuhusiana na wanachoandika kwenye mitandao ya jamii ili kujiepusha kusambaza jumbe za chuki na ukabila.

Ameongeza kuwa wamejitwika jukumu la kuwa mabalozi wa amani na heri njema na iwapo inahitajika kuongeza wazee kutoka jamii nyingine jimboni kwa ajili ya usalama watafanya hivyo.

Wakati uo huo, wazee hao wamepinga kuhusika kwa njia yoyote na machafuko hayo.

Sita hao ni pamoja na mwenyekiti wa baraza la jamii ya Borana Guracha Boru, mwenyekiti wa hazina ya CDF eneo bunge la Sakuu Guyo Bonaya na aliyekuwa diwani na mwanachama wa kamati ya uwiano Halakhe Waqo Golicha.

Wengine ni mwenyekiti wa baraza la jamii ya Gabra na aliyekuwa mkurugenzi wa elimu katika kaunti ya Marsabit Konchora Chepe, mwanachama wa bodi ya watoto wa kurandaranda na aliyekuwa mwakilishi wa Turbi/Bubisa Pius Yattani pamoja na mzee wa jamii Yattani Diba.

Viongozi wa kisiasa wametajwa kuwa chanzo kikuu cha mapigano ambayo yamegharimu maisha ya watu zaidi ya 15 katika muda wa miezi miwili pekee.

Washukiwa hao walimakatwa siku chache baada ya kamishna wa Marsabit Evans Achoki kuwaonya wanasiasa dhidi ya kuwachochea wananchi kupigana.

Subscribe to eNewsletter